Shirika la Habari la Hawza | Kwa kuzingatia yaliyotangulia, Ghaiba ya Imam Mahdi (a.s.) lilikuwa jambo la lazima na muhimu. Hata hivyo, kwa kuwa kila harakati na hatua za viongozi wakuu wetu zilikuwa kwa lengo la kuimarisha misingi ya imani na itikadi za watu, na kwa kuwa kulikuwa na hofu ya kwamba Ghaiba ya Imamu ingeleta madhara makubwa yasiyorekebishika katika dini ya kiislamu, basi kipindi cha Ghaiba kilianza kwa mpango makini na ufuatiliaji sahihi, na kikaendelea kwa utaratibu huo.
Miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwa Imam wa kumi na mbili (a.s.), suala la Ghaiba ya mtu huyo mkubwa lilianza kutajwa midomoni mwa watu na katika mikusanyiko ya Maimamu watoharifu (a.s.) na masahaba wao. Aidha, namna ya kuwasiliana kwa Imam Hadi na Imam ʿAskari (a.s.) na Mashia wao ilichukua sura mpya na ikawa yenye mipaka zaidi. Hali hii iliwafanya wafuasi wa madh-habu ya Ahlul-Bayt (a.s.) kuanza kuelewa kuwa katika mahitaji yao mengi ya kimwili na kiroho, hawakuwa na ulazima wa kufika mbele ya Imam anayehudhuria, bali waliweza kurejea kwa wale waliotajwa na Maimamu kama mawakili na watu wa kuaminika, na kutekeleza majukumu yao kwa njia hiyo.
Kwa kuuawa kishahidi Imam Hasan al-ʿAskari (a.s.) na kuanza kwa kipindi cha Ghaiba ya Hujjat ibn al-Hasan (a.s.), bado uhusiano kati ya Imam na Ummah haukukatikana kikamilifu. Bali watu waliendelea kuwasiliana na mola na kiongozi wao kupitia kwa mawakili maalumu wa Imam wa Zama (a.s.). Katika kipindi hicho, Mashia walizoea kuwa karibu zaidi na maulamaa wa dini, na walifahamu kuwa hata katika mazingira ya Ghaiba ya Imam, milango ya maarifa ya dini na wajibu wao haikufungwa.
Katika mazingira haya ya maandalizi, ndipo Ghaiba kubwa ya Bāqiyyatullāh (a.s.) ilipotokea na aina ya uhusiano wa moja kwa moja uliokuwepo awali kati ya Imam na Mashia wake ukakatika.
Ghayba ya Muda Mfupi (Ghaibat-a-Sughrā)
Kwa kuuawa kishahidi Imam Hasan ʿAskari (a.s.) mwaka 260 Hijria, kipindi cha Uimamu wa Imam wa kumi na mbili (a.s.) kilianza. Kuanzia hapo ndipo Ghaiba ya muda mfupi ilipoanza maarufu kama "Ghayba ndogo (Ṣughrā)" na ikaendelea hadi mwaka 329 Hijria, takriban miaka 70.
Sifa muhimu ya kipindi hiki ni kuwa watu walikuwa wakifanya mawasiliano yao na Imam Mahdi (a.s.) kupitia mawakili wake wa kipekee, waliokuwa wakiwasilisha ujumbe wa Imam kwa watu na kujibu maswali yao. Wakati mwingine, kwa kupitia mawakili hao, baadhi walibahatika kufika mbele ya Imam wao.
Mawakili hao wanne wa kipekee wa Imam (a.s.) ambao wote walikuwa ni maulamaa, wakubwa na walioteuliwa na Imam wa Zama (a.s.), ni kama ifuatavyo:
1. ʿUthmān ibn Saʿīd ʿAmrī, Alianza kazi ya uwakili tangu mwanzo wa Ghayba ya Imam na alifariki mwaka 267 Hijria. Alikuwa wakili wa Imam Hadi na Imam ʿAskari (a.s.) pia.
2. Muḥammad ibn ʿUthmān ʿAmrī, Mwanaye wakili wa kwanza. Aliteuliwa baada ya kifo cha baba yake na alifariki mwaka 305 Hijria.
3. Husayn ibn Rūh Nawbakhtī, Alihudumu kama wakili kwa miaka 21 hadi alipofariki mwaka 326 Hijria.
4. ʿAlī ibn Muḥammad al-Samorī, Alifariki mwaka 329 Hijria na kwa kifo chake, kipindi cha Ghaiba ndogo kilikamilika.
Mawakili wote hawa waliteuliwa na Imam ʿAskari (a.s.) na Imam Mahdi (a.s.) na walitambulishwa kwa watu. Katika kila kipindi cha uwakili, kila mmoja kabla ya kifo chake alimtangaza mrithi wake aliyechaguliwa na Imam Mahdi (a.s.).
Kama ilivyotajwa mwanzoni, mawasiliano haya na mawakili pamoja na kukutana kwa baadhi ya Mashia na Imam wao katika kipindi cha Ghaiba ndogo kulikuwa na athari kubwa katika kuthibitisha kuzaliwa kwa Imam wa kumi na mbili na kuwa hoja ya mwisho ya Mungu. Aidha, kipindi hiki kilikuwa maandalizi ya kufaa kwa kuanza kwa Ghaiba ndefu (Ghaybat-e-Kubrā).
Ghayba ya Muda Mrefu (Ghaybat-e-Kubrā)
Katika siku za mwisho za maisha ya wakili wa nne, barua kutoka kwa Imam Mahdi (a.s.) ilimfikia akisema:
«بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمنِ الرَّحِیمِ یَا عَلِیَّ بْنَ مُحَمَّدٍ السَّمُرِیَّ أَعْظَمَ اللَّهُ أَجْرَ إِخْوَانِکَ فِیکَ فَإِنَّکَ مَیِّتٌ مَا بَیْنَکَ وَ بَیْنَ سِتَّةِ أَیَّامٍ فَاجْمَعْ أَمْرَکَ وَلَا تُوصِ إِلَی أَحَدٍ فَیَقُومَ مَقَامَکَ بَعْدَ وَفَاتِکَ فَقَدْ وَقَعَتِ الْغَیْبَةُ التَّامَّةُ فَلَا ظُهُورَ إِلَّا بَعْدَ إِذْنِ اللَّهِ تَعَالَی ذِکْرُهُ وَ ذَلِکَ بَعْدَ طُولِ الْأَمَدِ وَقَسْوَةِ الْقُلُوبِ وَ امْتِلَاءِ الْأَرْضِ جَوْراً... .»
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Ewe ʿAlī ibn Muḥammad al-Samorī, Mwenyezi Mungu awaongezee thawabu ndugu zako wa kidini juu ya msiba wako; kwani baada ya siku sita utatoweka kwenye dunia hii. Basi jihusishe na mambo yako na usimwache mtu yeyote kuwa mrithi wako; kwa sababu kipindi cha Ghaiba kamili kimeanza, na hakutakuwa na kudhihiri [kwangu] isipokuwa baada ya amri ya Mwenyezi Mungu (jina Lake litukuzwe), na hilo litakuwa baada ya kipindi kirefu cha ukame wa nyoyo na kujazwa kwa dunia na dhuluma... . (Al-Ghaybah, Shaykh Ṭūsī, j.1, uk. 395)
Kwa hivyo, kwa kufariki kwa wakili wa mwisho maalumu wa Imam wa kumi na mbili mwaka 329 Hijria, kipindi cha Ghaiba ndefu maarufu kama Ghaybat-e-Kubrā kilianza, na kinaendelea hadi leo, hadi siku ambayo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, mawingu ya Ghaiba yataondoka na dunia itafaidika na mwangaza wa moja kwa moja wa jua linalong’aa la wilaya. "In shā’ Allāh."
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu: "Negin-e Āfarinish" baada ya kufanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako